MADAKTARI BINGWA WATOA MATIBABU BURE KWA WAZEE



Safina Sarwatt. Moshi.


TIMU  za madaktari bingwa  kutoka hospitali ya Jaffery Charitable Medical Services kwa kushirikiana na madaktari kutoka hospitali ya ya rufaa ya mkoa Kilimanjaro  Mawezi, wameanza kutoa huduma za matibabu ya afya bure  kwa wazee  500 kwa  Manispaa ya Moshi  kwa magonjwa yasiyoambukiza .

Hayo yameelezwa na Afisa Utawala wa hospitali hiyo, Faisal Kamal, Mjini hapa wakati wa zoezi la upimaji wa afya kwa wazee hao.

Kamal amesema  kuwa timu hiyo ya wataalamu imeona kuna haja kubwa kutoa huduma hiyo kwa kundi hilo la wazee kutokana na kwamba ni miongoni mwa kundi ambalo limekuwa likisahaulika katika jamii.

“Kundi la wazee ni kundi tete ambalo halina uwezo kifedha za kujitibu na pia wamekuwa wakikubwa na maradhi mbalimbali hivyo timu hii imeona umuhimu wa kuungana kwa pamoja kulisaidia kundi hili,’alisema Kamal

Mganga mkuu wa hospitali ya Jaffery Charitable Medical Services Dkt Sadick Daudi, amesema kuwa magonjwa ya yasiyopewa kipaumbele ambayo hayaambukizwi, yamekuwa yakilikumba kundi hilo la wazee na kuchangia
kwa vifo vya ghafla  kutokana na wengi wao kutokuwa na fedha za kujitibu.

Hata hivyo Dkt Daudi amesema kuwa miongoni mwa magonjwa ambayo wazee
hao wamepatiwa matibabu ni kisukari, shinikizo la damu pamoja na maradhi nyemelezi na kutoa ushauri wa kiafya kwa wazee.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Gelasius Byakanwa
ameipongeza hosptali ya Jaffery Charitable Medical Services, kwa mchango wake mkubwa wa kutoa huduma bure kwa wazee hao.

Aidha Byakanwa amesema kwamba serikali kupitia wizara ya afya itahakikisha wazee wanapatiwa matibabu bure kama vile ambavyo Sera ya afya inavyoelekeza.


EmoticonEmoticon