YANGA KUCHUKUA MILIONI 600 LEO ?

Kikosi cha Yanga tayari kimekamilisha maandalizi ya mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Wolaita Dicha kuelekea mechi itakayopigwa leo mjini Awassa, Ethiopia.

Meneja wa timu, Hafidh Saleh, ameeleza kuwa tayari kikosi kimeshakamilisha mazoezi yake na wako tayari kwa mtanange huo.

Saleh amesema wachezaji wote wako fiti kucheza leo na
hakuna aliye majeruhi.


Yanga itasonga mbele kwenye mashindano hayo mpaka hatua ya makundi endapo itatoa sare yoyote ile ama kuibuka na ushindi.

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Dar es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Kusonga mbele kwa Yanga kutaiwezesha kutwaa zaidi ya milioni 600 za kitanzania kama ilivyo utaratibu wa CAF kutoka kitita hicho cha pesa.

BARBARA BUSH AFARIKI AKIWA NA MIAKA 92


Barbara Bush na mumewe aliyekuwa rais wa Marekani George HW Bush
Barbara Bush, mke wa aliyekuwa rais wa zamani wa Marekani na mwanaharakati amefariki akiwa na umri wa miaka 92.
Ndiye aliyekuwa nguzo ya kisiasa ya marais wawili wa taifa hilo akiwemo mumewe George HW Bush na mwanae George W Bush.


Bi Bush ambaye alikuwa mke wa rais kutoka 1989 hadi 1993 amekuwa akidorora kiafya kwa muda sasa na alikuwa amekataa kupatiwa matibabu zaidi.


Risala za rambirambi zimetumwa nchini Marekani kutoka maeneo tofauti duniani.
Mumewe aliye na umri wa miaka 93 ndiye rais aliyeishi kwa muda mrefu nchini Marekani.


Mwanao George Bush alichaguliwa mwaka 2000 na kuhudumu kwa miula miwili kama rais wa 43 wa Marekani.

CELTA VIGO YAIBANIA FC BARCELONA NJE NDANI LA LIGA

Barcelona imeendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kuwa na alama zake 83 kati ya michezo 33 iliyocheza.
Barcelona ililazimisha sare ya mabao 2-2 ikiwa ugenini katika Ligi Kuu Spain,huku mabao yake yakifungwa na Dembele dakika ya 36 na la pili likitiwa kimiani na Alcacer mnamo dakika ya 64.
Kikosi hicho kilicheza kikiwa pungufu kuanzia dakika ya 71 baada ya Sergi Roberto kulimwa kadi nyekundu.
Celta Vigo imekuwa timu pekee ambayo imeshindwa kupoteza mbele ya Barcelona msimu huu baada ya kuilazimisha Barcelona kupata matokeo ya sare katika michezo yote miwili ya ligi.
Hiyo imekuwa ni rekodi kwa Celta ukiangalia baadhi ya vigogo wengine kama Atletico na Real Madrid tayari wameshapokea vichapo kutoka kwa vinara hao wa ligi msimu huu.

WAKAZI WA BOLISA KUSOGEZEWA HUDUMA YA ELIMU KARIBU

Wananchi wa kata ya Bolisa wanatarajia kujengewa shule mpya ya sekondari ya kata ili kuondokana na  tatizo la umbali kwa wanafunzi  wa kata hiyo, amebainisha na Mkurugenzi wa Mji Kondoa Bw. Khalifa Kondo alipokuwa akijibu swali wakati wa mkutano wa wananchi  wa kata ya Bolisa na Mkuu wa Mkoa  alipofanya ziara ya kujitambulisha wilayani humo hivi karibuni.  

"Shule ya Gubali imeshughulikiwa na wananchi wa kata ya Gulisa kabla ya kugawanywa kuwa kata mbili lakini kwasasa kata ipo kata ya Kolo tunaomba kujua mipaka ya kata hizi mbili ili shule ya Gubali ibaki Bolisa".aliuliza bwana Abubakari Mussa.

Akifafanua Bwana Kondo alisema kuwa ni kweli shule hiyo ipo lakini kutokana na mazingira ya shule hiyo wameanza kupata fedha za kujenga mabweni  katika shule ya  Sekondari Gubali  kwa ajili ya wanafunzi  kutoka nchi nzima na si Kolo tu. 

Kondo aliendelea kufafanua kuwa kutokana na mipango hiyo wilaya imejipanga kujenga shule mpya ya Sekondari  kwa ajili ya wananchi wa kata ya Bolisa kwa ajili ya kuwasogezea huduma wananchi kwa ukaribu kwani ndio lengo la serikali ya awamu ya tano.

Aidha aliongeza kuwa  Rais amemwagiza Waziri wa ujenzi  kuiachia wilaya  majengo yaliyokuwa yanatumiwa na kampuni ya ujenzi wa barabara eneo la Kolo ili yatumike kwa ajili ya kuanzisha shule ya sekondari kwa wanafunzi wenye vipaji maalum toka nchi nzima.

Baada ya ufafanuzi huo Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Mahenge alipongeza mpango huo na kuwataka kuutekeleza kwa ushirikiano ili wananchi wapate huduma inayostahili.

Shule ya Sekondari Gubali ni shule ya Sekondari iliyopo katika kata ya Kolo ikihudumia wananchi wa kata hiyo na kata ya Bolisa ambapo imejengwa juu ya mlima hali inayowapa shida wanafunzi kufika shule.



 Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt. Nobility Mahenge kushoto akimuonyesha kitu Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mh. Sezaria Makota wakati wa ziara yake wilayani humo.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Mwalimu Kibasa akijibu swali kwenye mkutano wa wananchi na mkuu wa Mkoa katika kata ya Bolisa.



 Mkurugenzi wa Mji Kondoa Khalifa Kondo akifafanua jambo kwenye mkutano wa wananchi na Mkuu wa mkoa

TAKUKURU YATANGAZA DAU LA MIL 10 KUPATIKANA KWA MHASIBU WA TAASISI HIYO

Naibu mkurugenzi wa Takukuru Bregedia John Mbungo

Taasisi ya kuzuia na kupamabana na rushwa nchini (TAKUKURU) imetengaza zawadi nono ya shilingi milioni kumi kwa mtu atayewezesha kupatikana kwa aliyekuwa mhasibu wa taasisi hiyo, Godffrey Gugai anayedai kuwa na ukwasi mkubwa wa fedha na mali isiyolingana na kipato chake halali akiwa kama mtumishi wa umma.

 Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Bregedia John Mbungo amesema, baada ya kuchunguza na kutoa taarifa ya awali walimuita Gugai na kumuhoji ambapo alionyesha ushirikiano wa kujibu hoja hizo zinazomkabili na kuwa na mali nyingi kuliko kipato chake.

Amesema, kwa mujibu wa kifungu cha 27 cha sheria ya Kuzuia na kupaambana na Rushwa ni kosa la jinai kwa afisa wa serikali au mtumishi wa umma kuwa na mali nyingi au maisha ambayo yanazidi kipato chake bila ya kuwa na maelezo yoyote anayoelezea mali zile amezipata wapi au kwa namna gani.

“Bwana Gugai aliweza kujikusanyia mali nyingi ambazo awali tulijaribu kumuuliza na alielekea kuonyesha ushirikiano lakini baadae alipoona kwamba hana maelezo ya namna gani amezipata zile mali akapotea. tumeendelea kumtafuta na taarifa ambazo tumekuwa tukizipata amekuwa ni mtoro amekimbilia nje ya nchi kupitia njia ambazo siyo rasmi” amesema Bregedia Jenerali Mbungo.

Mhasibu huyo anamiliki maghorofa saba, nyumba za kawaida tisa, magari matano na pikipiki pamoja na viwanja 37.
 Amesema ni kosa kubwa kwa mtumishi wa umma kutumia ofisi yake kujipatia mali  nje ya kipato akipatacho ni kosa, aliwahi kuchukuliwa maelezo, alipogundua hana maelezo sahihi akaamua kukimbia.

Maghorofa, nyumba za kawaida na viwanja vya mhasibu huyo viko kwa mtawanyiko katika maeneo mbalimbali nchini yakiwamo ya ghali karibu na bahari, Kigamboni na Mbweni jijini Dar es Salaam na pia Bagamoyo mkoani Pwani. Kwingineko kuliko na mali hizo ni Kinondoni (Dar), Musoma, Nyegezi, Kiseke jijini Mwanza, Arusha na Tanga.

Hata hivyo, mali za Gugai zimewekewa zuio la mahakama na mawakala wake na watu wengine wote wanaomwakilisha wamezuiwa kuuza au kuhamisha umiliki au kuweka dhamana mali zote zilizowekewa zuio.


 Pia Msajili Msaidizi wa magari ameagizwa asiruhusu uhamishaji wa umiliki wa vyombo vya moto vilivyowekewa zuio mpaka mahakama itakapoelekeza vinginevyo.

DR KIGWANGALLA AKABIDHI VIFAA TIBA KIBAHA MJINI

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamisi Kigwangalla amekabidhi jumla ya vifaa 831 vyenye thamani ya jumla ya Shilingi milioni 400, kwa kituo cha Afya Mkoani Kibaha Mjini, vifaa vilivyotolewa na Mbunge wa jimbo hilo, Mh. Silvestry Koka.

Awali kabla ya kukabidhi vifaa hivyo, Dk. Kigwangalla alipata wasaha wa kukagua maeneo ya majengo ya Kituo hicho cha Afya huku akbaini mambo mbalimbali aliyoagiza yafanyiwe kazi ili kituo hicho kiweze kuwa Hospitali ya Wilaya pindi itakapokamilisha vigezo.

Wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Dk. Kigwangalla alipongeza juhudi za Mh. Koka kwa kujali wananchi wake kwani hadi kuweza kupata vifaa hivyo aliweza kutumia maarifa na ukaribu wake na wananchi wake hivyo kufika kwa vifaa hivyo vitakuwa faraja kubwa kwa Wanakibaha na wananchi wote wa maeneo jirani.

“Nampongeza Mbunge Koka kwa kuwaletea vifaa hivi. Kwani ni vizuri na vitakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Kibaha na maeneo yake ya jirani. Nakupongeza sana sana” alieleza Dk. Kigwangalla wakati wa tukio hilo la kukabidhi vifaa hivyo.

Aidha, aliwataka wananchi wa Kibaha mjini waweze kuwa karibu na Mbunge wao na wamwamini kwani anawajali ndio maana anawatumikia kwa kila njia ikiwemo kuwaletea maendeleo kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kibaha Mjini Mh. Silvestry Koka amemshukuru Naibu Waziri Dk. Kigwangalla kwa kuweza kufika na kujionea Kituo hicho sambamba na kukabidhi vifaa huku akimuomba kuendelea kufika mara kwa mara kujionea mipango ya Afya jimboni humo.

“Leo hiii najisikia faraja kwa vifaa hivi kuweza kufika  hapa jimboni kwangu kutoka nchini Marekani. Nawaomba vitumike kwa uangalifu mkubwa sana na viweze kuwa msaada kwetu” alieleza Mh. Koka.

Awali alieleza kuwa, kiasi cha shilingi milioni 32  fedha zilizotolewa na Halmshauri ya mji wa Kibaha ziweza kusaidia usafirishaji wa vifaa hivyo kutoka nchini Marekani huku yeye kama Mbunge akitumia gharama ya shilingi milioni 12 kwa ajili ya kuwaleta wataalam kwa ajili ya ukaguzi na kuvifunga vifaa hivyo.

Mbunge huyo ameeleza kuwa, vifaa hivyo vitagawia katika zahanati na vituo vyote vilivyopo mjini Kibaha na maeneo mengine yenye uhitaji.

KAPOMBE AAHIDI MAKUBWA SIMBA

Beki mpya wa Simba, Shomari Kapombe anaamini Simba itafanya vizuri msimu ujao.
Kapombe amesema Simba imeanza kuonyesha kweli inataka kudumisha kikosi chake, hivyo anaamini itafanya vizuri.
“Ukiangalia usajili unaofanyika sasa na kikosi kilichopo, hakuna ubishi kwamba Simba itakuwa na kikosi kizuri.
“Kikosi kizuri maana yake ni kwamba, tuna nafasi ya kufanya vizuri na litakalofuata ni maandalizi mazuri na ushirikiano wa kutosha,” alisema Kapombe ambaye amerejea Simba.
Kapombe amesaini kuichezea Simba kwa mkataba wa miaka miwili.