SIMBA KUIFUNDISHA TENA ADABU AZAM FC SEPTEMBER 8 ?


Mabingwa wa ligi kuu ya vodacom Simba itamenyana na Azam katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 8, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.
 
Katika mechi ya jana dhidi ya Timu ya Mathare united ya Kenya makipa wa akiba wa klabu ya Simba, Albert Mweta na Hamadi Waziri jana walionyesha viwango vizuri katika mchezo wa kirafiki wa klabu hiyo dhidi ya Mathare United ya Kenya,kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
 
Mweta aliyesajiliwa msimu uliopita kutoka Toto African ya Mwanza jana alianza na kumaliza dakika 45 bila kufungwa, kabla ya kufungwa bao moja kipindi cha pili, tena baada ya mabeki Paschal Ochieng na Juma Nyosso kuchanganyana.
Akiwa langoni, Mweta aliokoa hatari kadhaa na kuonyesha kwamba ni kipa aliye tayari hata mechi kubwa.
Alipoingia Hamadi aliyesajiliwa msimu huu kutoka JKT Oljoro ya Arusha, naye pia alionyesha kiwango kizuri na kuokoa michomo kadhaa ya hatari.
Makipa hao, walidaka jana kwa sababu kipa namba moja wa Simba, Juma Kaseja alikuwa mgonjwa.
Katika mchezo huo, bao la penalti dakika ya 81 lililofungwa na kiungo Kiggi Makassy, lilitosha kuipa Simba ushindi wa mabao 2-1, kabla ya kuingia kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC wiki mbili zijazo mjini Dar es Salaam.
Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao na kipindi cha pili, Simba SC inayofundishwa na Mserbia, Milovan Cirkovick ilipata bao la kuongoza dakika ya 53, mfungaji mshambuliaji kutoka Ghana, Daniel Akuffo aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Amir Maftah.
 
Mathare walisawazisha bao hilo dakika ya 68, mfungaji Daniel Mwaura aliyeipasua ngome ya Simba SC, iliyokuwa ikiongozwa na Paschal Ochieng na Juma Nyosso.
Beki wa Mathare alimuangusha kwenye eneo la hatari, Uhuru Suleiman dakika ya 81 na refa akaamuru ipigwe penalti, iliyopachikwa kimiani kiufundi kwa guu la kushoto la Kiggi Makassy.
Simba ilicheza vizuri mechi hiyo, leo hii Haruna Moshi ‘Boban’ akirudishwa katika nafasi ya kiungo baada ya kupatikana kwa washambuliaji halisi. Alicheza kwa utulivu, akigawa vizuri mipira na hata kuwapokonya mipira viungo wa timu ya Mathare united.
Dakika za mwishoni ilishuhudiwa Boban akipitia mpira kwa nguvu miguuni mwa mshambuliaji wa Mathare, baada ya Maftah kupitwa, kuashiria kwamba kijana amebadilika si Yule wa kukaba kwa macho.

Juma Kaseja na Mrisho Ngassa hawakushiriki kabisa mechi hiyo kwa sababu walikuwa wagonjwa na Keita alimpisha Nyosso baada ya kuumia.
 
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba kilikuwa; Wilbert Mweta/Hassan Waziri, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah/Paul Ngalema, Paschal Ochieng, Komabil Keita/Juma Nyosso, Salum Kinje/Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Mwinyi Kazimoto/Haruna Shamte, Haruna Moshi, Felix Sunzu, Abdallah Juma/Amri Kiemba na Daniel Akuffo/Uhuru Suleiman.


EmoticonEmoticon