MAAFANDE WA JKT OLJORO YA ARUSHA KUMSAJILI BEKI KISIKI JUMA JABU


Uongozi wa Maafande wa timu ya JKT Oljoro ya jijini Arusha umeanza mazungumzo na beki wa Mabingwa wa ligi kuu ya Vodacom Wekundu wa Msimbazi Simba, Juma Jabu kwa lengo la kumsajili kwa msimu ujao wa ligi kuu ya Vodacom.

Jabu aliyemaliza mkataba wake na mabingwa wa Tanzania, Simba hivi karibuni aliweka bayana kwamba anasaka timu ya kuichezea kwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom.


Akizungumza na Sunrise Radio, Katibu mkuu wa JKT Oljoro, Alex Mwamgaya alisema kuwa wako katika mazungumzo na mchezaji huyo kwa lengo la kuimarisha safu yao ya ulinzi katika msimi ujao wa ligi kuu.

Kwa upande wake Juma Jabu amesema yupo tayari kuichezea timu yoyote na kudai yeye haangalii ni timu gani atachezea bali kama watakubaliani katika mazungumzo yuko tayari kuichezea timu hiyo.

Jabu ni miongoni mwa mabeki bora katika kikosi cha Simba walioisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu wa 2011-2012.


Mbali na Jabu, wachezaji wengine wanaotegemea kuondoka Simba kwa sababu ya kumaliza mkataba ni pamoja na Juma Nyoso, Uhuru Seleman, Gervais Kargo na wale waliokuwa wakicheza kwa mkopo Amri Kiemba na Haruna Shamte.


EmoticonEmoticon