Michuano
ya Copa Coca-Cola ngazi ya Taifa inaanza kutimua vumbi Juni 24 mwaka
huu kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani huku pambano la ufunguzi
likiwa kati ya Kigoma na Lindi litakalofanyika kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Upangaji
ratiba (draw) umefanyika leo (Juni 7 mwaka huu) kwenye ofisi za
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kushuhudiwa na waandishi
wa habari, makocha wa timu za mikoa za Copa Coca-Cola na wadhamini
kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola.
Makocha
35 wa timu za Copa Coca-Cola kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na
Visiwani wako kwenye kozi ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) inayoendeshwa na wakufunzi Ulric Mathiot wa FIFA kutoka
Seychelles na wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Sunday
Kayuni wa Tanzania.
Mikoa
28 ya kimpira ya Tanzania itashiriki katika mashindano hayo na
imegawanywa katika makundi manne ya timu saba saba. Baadaye timu
zitapambana katika hatua ya robo fainali, nusu fainali na fainali
itakayofanyika Julai 15 mwaka huu.
Kundi
A lina timu za Arusha, Ilala, Kigoma, Kusini Pemba, Lindi, Rukwa na
Ruvuma. Kundi B ni Iringa, Kaskazini Pemba, Manyara, Mjini Magharibi,
Morogoro, Mwanza na Tanga. Dodoma, Kaskazini Unguja, Kinondoni, Mara,
Mbeya, Mtwara na Temeke ziko kundi C wakati kundi D ni Kagera,
Kilimanjaro, Kusini Unguja, Pwani, Shinyanga, Singida na Tabora.
Viwanja
vitakavyotumika katika mashindano hayo ambapo mechi zitakuwa zikichezwa
asubuhi (saa 2.30) na jioni (saa 10.00) ni Uwanja wa Karume na
Tanganyika Packers (Kawe) kwa Dar es Salaam. Viwanja vya Mkoa wa Pwani
ni Tamco na Nyumbu. Timu zote katika mashindano hayo zitacheza katika
viwanja hivyo.
Mbali
ya Kigoma na Lindi, mechi nyingine za ufunguzi Juni 24 mwaka huu ni
kundi B Morogoro na Manyara (saa 2.30 asubuhi Uwanja wa Kawe), kundi C
ni Temeke na Kinondoni (saa 2.30 asubuhi Uwanja wa Nyumbu) na kundi D ni
Kilimanjaro na Kusini Unguja (saa 2.30 asubuhi Uwanja wa Tamco).
Wachezaji wanaotakiwa kushiriki kwenye michuano hiyo ya umri chini ya miaka 17 ni wale waliozaliwa kuanzia Januari 1, 1996.
EmoticonEmoticon