WASHIRIKI WA BSS WATAKIWA KUJIENDELEZA BAADA YA SHINDANO KUMALIZIKA

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeridhishwa na shindano la Bongo Star Search huku washiriki watakiwa kujiendeleza wenyewe badala ya kutegemea kusaidiwa na mradi huo pindi shindano linapomalizika.

 Kauli hiyo imetolewa na mratibu wa BSS kutoka Basata Vicky Temu wakati akichangia mada katika mkutano uliowashirikisha BSS na wadau wa sanaa nchini.

 Vicky alisema kuwa wasanii hao wanatakiwa kutambua kuwa uhusiano kati ya BSS na wasanii hao unamalizika mara baada ya shindano kumalizika hivyo wanatakiwa kutumia vyema elimu ya muziki waliyoipata wakiwa ndani ya shindano hilo kujiendeleza zaidi.

 Hata hivyo alimtaka mwandaaji wa shindano hilo Ritha Paulsen kuwaendeleza wasanii hao ikiwa ni pamoja na kuingia nao mikataba na studio za kurekodia muziki kwa lengo la kuwaendeleza zaidi watakaofanya vyema pindi shindano hilo linapomalizika.

 Naye mwandaaji wa shindano hilo Rita Paulsen, amewataka waandishi wa habari pamoja na watangazaji wa redio na luninga kuwasaidia wasanii hao wa BSS badala ya kuwakatisha tamaa ya kusonga mbele kimuziki.

 Rita amesema kuna wadau mbalimbali katika vyombo vya habari na sanaa kiujumla ambapo wanawakatisha tamaa wasanii watokanao na mradi wa BSS kwa kutotaka kuwasaidia kuwatangaza nyimbo zao ama kuwatangaza wao kama wao.

 Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Kitengo cha Matukio cha Basata, Malimu Mashili amesema kuwa baraza hilo haliwezi kutoa kibali kamili kabla halijapata mwelekeo wa shindano la mwaka huu ili kama chochote kikiharibika ni baraza ndio litahusika.

 Kikao kilimalizika huku Basata ikiwa imemtaka Madam Rita kuwasilisha bajeti inayotaja zawadi, na gharama nyinginezo licha ya kuwa Rita aliwataka wampatie kibali kamili ili aweze kusaini mkataba na mdhamini wake lakini hata hivyo alisema kuwa suala la kutaja zawadi ni mapema mno kwa kuwa wadhamini wengine hujitokeza shindano likiwa limenza.

 Mtafaruku mwingine uliibuka katika suala la upatikanaji wa majaji wa shindano hilo ambapo Basata ilimtaka Rita kuwapelekea majina ya watu watano ili iweze kuwachagua watatu kati yao huku ikisisitiza kuwa huo ni utaratibu wa kawaida.

 Akionesha kushangazwa na utaratibu huo Rita amesema kuwa anapenda kuwatumia majaji wake wale wale kwa kuwa ndio ameshawajengea hisia nzuri kwa washabiki wa BSS na huvutia kipindi hivyo kuwabadilisha sio haki.


EmoticonEmoticon