WAENDESHA BODABODA WAPEWA MAFUNZO

Serikali yaombwa kufungua benki ya viwanda vidogovidogo itakayowawezesha wajasiriamali na vikundi rasmi kwa lengo la kuviwezesha vikundi hivyo kupata mikopo yenye riba nafuu katika shughuli zao za uzalishaji kwa ajili ya maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Hayo yameelezwa na mkurugenzi mkuu wa taasisi isiyokuwa ya kiserikali bwana Respicius Timanywa,inayojulikana kwa jina la ,Anti-Porverty and Invironmental Care ,(APEC) inayotoa mafunzo ya usalama barabarani kwa waendesha bodaboda na kusisitiza wasitegemee kuendesha bodaboda pekee ila wanayofursa nyingine ya kuanzisha miradi ya ufyatuaji matofali, ufugaji wa kuku, mashine za kutotoa vifaranga pamoja na viwanda vya uzalishaji wa maji na uchimbaji wa visima.

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wa mafunzo hayo bwana Moses Mafie katika Wilaya ya Arumeru Kata ya Kikatiti Kijiji cha Sakila wamebainisha kuwa miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ni pamoja na kukabwa na kupokonywa pikipiki zao.

 
Ameongeza pia abiria kukataa kuvaa kofia ngumu,magari makubwa kuwachomekea wakiwa barabarani sambamba na mwamko mdogo wa baadhi ya madereva kutokushiriki mafunzo ya usalama barabarani ambao hupelekea kuonekana kuwa hawana elimu ya usalama barabarani.

 Katika hotuba yake mgeni rasmi SSP Nuru Selemani ambaye ni mkuu wa kikosi usalama cha barabarani mkoa wa Arusha,tafsiri ya serikali kuruhusu usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda ni kurahisisha usafiri,kuongeza ajira kwa vijana.

“Lengo kuu la kuruhusiwa kwa usafiri wa pikipiki nchini ni wananchi wetu wasipate taabu ya usafiri,vijana wetu waweze kujiajiri na kujipatia kipato cha kujikimu kimaisha na kuepuka kukaa hovyo vijiweni bila kazi” alisisitiza Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Arusha.

 
Aidha amewataka wahitimu hao kuwa mfano mzuri wa kutoa elimu kwa wenzao hata kwenye jamii wanamoishi huku akiwasisitizia kufuata alama zote za usalama barabarani ili kuepusha ajali .

“Zingatieni alama zote za usalama barabarani,yatumieni mafunzo yenu kuwalinda na wengine,epukeni ulevi maana ajali nyingi zinasababishwa na ulevi kwa baadhi ya madereva wa vyombo vya moto,vaeni kofia ngumu pamoja na abiria wenu wapeni kofia ngumu,dereva bora na makini ni yule anayekifahamu chombo chake,na kuzingatia sheria za usalama barabarani”alisisitiza SSP Nuru Selemani.

Takwimu za ajali kuanzia januari hadi septemba mwaka huu zilizoripotiwa ni 445 hivyo amewataka wahitimu kufanyia kazi mafunzo hayo kwa vitendo ili kuweza kupunguza ajali za barabarani.



Katikati ni SSP Nuru Selemeni ,Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Arusha, wa kulia ni Mkurugenzi wa (APEC) Respicius Timanywa kushoto ni muwakilishi wa wa DTO Arumeru Godbless Kasaini.

SSP Nuru Selemani Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Arusha.







EmoticonEmoticon