DR KIGWANGALLA AKABIDHI VIFAA TIBA KIBAHA MJINI

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamisi Kigwangalla amekabidhi jumla ya vifaa 831 vyenye thamani ya jumla ya Shilingi milioni 400, kwa kituo cha Afya Mkoani Kibaha Mjini, vifaa vilivyotolewa na Mbunge wa jimbo hilo, Mh. Silvestry Koka.

Awali kabla ya kukabidhi vifaa hivyo, Dk. Kigwangalla alipata wasaha wa kukagua maeneo ya majengo ya Kituo hicho cha Afya huku akbaini mambo mbalimbali aliyoagiza yafanyiwe kazi ili kituo hicho kiweze kuwa Hospitali ya Wilaya pindi itakapokamilisha vigezo.

Wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Dk. Kigwangalla alipongeza juhudi za Mh. Koka kwa kujali wananchi wake kwani hadi kuweza kupata vifaa hivyo aliweza kutumia maarifa na ukaribu wake na wananchi wake hivyo kufika kwa vifaa hivyo vitakuwa faraja kubwa kwa Wanakibaha na wananchi wote wa maeneo jirani.

“Nampongeza Mbunge Koka kwa kuwaletea vifaa hivi. Kwani ni vizuri na vitakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Kibaha na maeneo yake ya jirani. Nakupongeza sana sana” alieleza Dk. Kigwangalla wakati wa tukio hilo la kukabidhi vifaa hivyo.

Aidha, aliwataka wananchi wa Kibaha mjini waweze kuwa karibu na Mbunge wao na wamwamini kwani anawajali ndio maana anawatumikia kwa kila njia ikiwemo kuwaletea maendeleo kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kibaha Mjini Mh. Silvestry Koka amemshukuru Naibu Waziri Dk. Kigwangalla kwa kuweza kufika na kujionea Kituo hicho sambamba na kukabidhi vifaa huku akimuomba kuendelea kufika mara kwa mara kujionea mipango ya Afya jimboni humo.

“Leo hiii najisikia faraja kwa vifaa hivi kuweza kufika  hapa jimboni kwangu kutoka nchini Marekani. Nawaomba vitumike kwa uangalifu mkubwa sana na viweze kuwa msaada kwetu” alieleza Mh. Koka.

Awali alieleza kuwa, kiasi cha shilingi milioni 32  fedha zilizotolewa na Halmshauri ya mji wa Kibaha ziweza kusaidia usafirishaji wa vifaa hivyo kutoka nchini Marekani huku yeye kama Mbunge akitumia gharama ya shilingi milioni 12 kwa ajili ya kuwaleta wataalam kwa ajili ya ukaguzi na kuvifunga vifaa hivyo.

Mbunge huyo ameeleza kuwa, vifaa hivyo vitagawia katika zahanati na vituo vyote vilivyopo mjini Kibaha na maeneo mengine yenye uhitaji.


EmoticonEmoticon