
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya tukio la jana,
Jumapili, Mei 5, 2013 la mlipuko kwenye Kanisa Katoliki la Mt. Joseph
Mfanyakazi la Olasiti Jijini Arusha. Tukio hilo la kigaidi
limesababisha...
Watu wawili kupoteza maisha hadi hivi sasa na majeruhi zaidi ya 60
Rais
Kikwete analaani vikali shambulio hilo lililofanywa na mtu au watu
katili, waovu na wenye dhamira mbaya na nia mbaya kwa Tanzania na watu
wake.
Rais Kikwete ameagiza
vyombo vya usalama nchini kumsaka mtu au watu waliohusika na kitendo
hicho kiovu na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Vile vile Rais Kikwete amewataka wananchi wote kuwa watulivu wakati Serikali na vyombo vyake inaendelea kufuatilia tukio hili.
"Tutawasaka
popote walipo na kupambana nao bila huruma. Aidha, tutakabiliana na
aina yoyote ya uhalifu nchini iwe ni ugaidi au aina yoyote ya uhalifu wa
namna hiyo au wa namna nyingine, uwe na chimbuko lake ndani ya nchi ama
nje ya nchi yetu.
"Kamwe hatutakubali kuwaacha wavuruge amani na usalama wa Tanzania na watu wake" amesema
Rais ambaye anaamini kuwa Serikali, kwa msaada na ushirikiano wa
wananchi, watu hao watapatikana na kuadabishwa ipasavyo.
Aidha,
Rais Kikwete anatoa rambirambi za dhati ya moyo wake kwa wafiwa na wale
wote ambao wamejeruhiwa katika tukio hilo. Anaungana nao katika machungu
na msiba. Rais pia anawaombea wote walioumia katika tukio hili wapate
nafuu ya haraka na waendelee na shughuli zao za ujenzi wa taifa.
Rais
Kikwete vilevile anatoa pole nyingi kwa viongozi na waumini wa Kanisa
Katoliki kwa tukio hili la kusikitisha na kuvurugika kwa ibada na
shughuli yao muhimu ya uzinduzi wa Kanisa lao.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
5 Mei, 2013
EmoticonEmoticon