VILABU VYASUBIRIWA KUTOA KAULI JUU YA KUVUNJWA MKATABA WA TFF NA VODACOM


Angetile Osiah



SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema kuwa lipo tayari kuvunja mkataba na wadhamini wakuu wa Ligi Kuu, Kampuni ya Vodacom iwapo vilabu vitakuwa tayari kuvunjwa kwa mkataba huo.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema jana kuwa, kama klabu zitaridhia uamuzi huo, basi shirikisho lake halitasita kufanya hivyo.


Osiah alisema mawasiliano mabovu kati ya Kamati ya Ligi na wenzao wa klabu, kulipelekea timu ya African Lyon kuingia mkataba na Zantel, uamuzi ambao ni kinyume na kipengele cha wadhamini Vodacom kinachokataza wapinzani wao kuingia.

"Klabu zilipendekeza kupewa milioni 10, lakini Vodacom walikataa na kusema uwezo wao ni Sh1.6 bilioni kwa mwaka," alisema.

Pia klabu zilipendekeza kama Vodacom haitaki mshindani wake kuingia, basi watoe dola kwa kuangalia soko la fedha za kigeni zinavyopanda na kushuka, jambo ambalo pia wadhamini hao walikataa.

Kuhusu kusaini mkataba wa Vodacom, Osiah alisema:"Mkataba nimesaini mimi baada ya kupata idhini kutoka kwa wawakilishi wa klabu. Tulikaa na klabu na kupitia vipengele, Rais (Leodegar Tenga) aliwaambia kuwa vifaa vitachelewa kutokana na kutosainiwa mkataba mapema."


Wakati hayo yakiendelea, Vodacom imesema inajisikia faraja kuendelea kudhamini Ligi Kuu kwa miaka mitatu mingine pamoja na kuwapo kwa malumbano kati ya vilabu na TFF.

Vodacom Tanzania ilisaini mkataba wa miaka mitatu na TFF Jumanne iliyopita, lakini klabu zinapinga baada ya kuondelewa kipengele cha upekee (exclusivity), ambacho kinazuia kampuni shindani na Vodacom kudhamini klabu au ligi hiyo.

Mkuu wa Mawasiliano na Masoko wa Vodacom, Kelvin Twissa alisema jana kuwa kusainiwa kwa mkataba huo kumetokana na makubaliano kati ya TFF na Kamati ya Ligi na hasa baada ya kuondoa kipengele hicho.

Twissa alisema kwa sasa hawafikiri kuvunja mkataba huo pamoja na kuwapo kwa malumbano hayo.

Vodacom inatarajia kutoa Sh1.6 kwa mwaka kudhamini ligi hiyo, huku klabu zikipata Sh70 milioni za nauli na bingwa kupata Sh70 milioni.


EmoticonEmoticon