TOM OLABA APEWA KISOGO MTIBWA SUGAR

KOCHA wa Mtibwa Sugar, Tom Olaba aliyemaliza mkataba wake tangu Juni amesema yupo katika hali ya sintofahamu kutokana na ukimya wa viongozi wa klabu hiyo.

Tom Olaba alisema kuwa hatua ya kutojua hatma yake kumepelekea ashindwe kuandaa programu ya kikosi cha timu yake kwaajili ya msimu ujao.

"Kimsingi hakuna kilichofanyika kwetu, timu haijafanya maandalizi yoyote mpaka sasa, isitoshe mkataba wangu ulimalizika tangu Juni na mpaka sasa uongozi haujaniambia chochote,"alisema Olaba na kuongeza:

"Labla ukimuuliza Jamal Bayser(meneja Mtibwa Sugar)anaweza kukueleza kitu kuhusu timu na mipango yote, kwa kweli jambo hili limenifanya nishindwe pia kuandaa programu zangu,".

Akizungumzia madai hayo, Baiyser alisema uongozi wa klabu yake utamtangaza kocha wa timu hiyo muda wowote kuanzia sasa na kuongeza kuwa maandalizi rasmi ya msimu ujao kwa klabu yake yataanza Julai 15.

"Tunamtangaza kocha atakayefundisha Mtibwa wakati wowote kuanzia sasa, siwezi kusema atakuwa Olaba au mwingine, lakini atajulikana hivi karibuni.

"Zaidi ya hapo maandalizi rasmi ya kikosi chetu kwaajili ya msimu ujao yataanza Julai 15,"alisema Bayser.


EmoticonEmoticon