BAYI APATA SHAVU LA TOC

                                           Filbert Bayi

KAMATI ya Olimpiki Tanzania (TOC), imeelezea kuwa na imani na utendaji wa Katibu Mkuu wake, Filbert Bayi, tofauti na shutuma ambazo zimekuwa zikitolewa na mdau wa michezo, Wilhelm Gidabuday.

Hivi karibu, Gidabuday amekuwa akitoa madai mbalimbali yakiwamo ya ubadhirifu na utendaji mbovu ambapo tatizo ni Bayi, huku pia akidai katibu huyo kaiweka kambi nyumbani kwake Kibaha, badala ya kuwekwa eneo lenye baridi hususan Arusha.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Rais wa TOC, Ghulam Rashid, alisema tuhuma hizo zinazotolewa na Gidabuday si za kweli, kwani kamati hiyo iko wazi kiutendaji na hesabu zake za mapato na matumizi hufanyiwa ukaguzi wa kitaalamu.


Rashid alifafanua kuwa, fedha wanazopokea kutoka Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa, (IOC), zinatokana na kuandika ‘proposal’ jinsi zitakavyotumika na ikiridhiwa ndipo hupewa na hutakiwa mrejesho.


Aliongeza kuwa, katika kuelekea michezo ya Olimpiki London, walipeleka maombi Olympic Solidarity, na kupewa dola 100,000 ambako kwanza walitanguliziwa dola 25,000, ambako zilitumika kwa maandalizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na yale ya kufuzu kwa michezo ya riadha, judo na bgymi za ridhaa.


Mchanganuo wa fedha hizo ni mazoezi ya judo huko Zanzibar na Dar es Salaam kwa siku 30 na safari ya Morocco, riadha mazoezi siku 114, ngumi mazoezi siku 107, vifaa na safari ya Morocco, ambako zilitumika dola 90,903.13 huku baki ikiwa ni dola 9,096.87 ambazo zitatumika kwa malazi, posho na usafiri wa wanamichezo watakaporejea kutoka London.


Kuhusiana na kambi kuwekwa Kibaha, Rais huyo alisema ulikuwa ni uamuzi wa Kamati ya Utendaji na si Bayi, ambapo pia huwa na wanawasiliana na Mkurugenzi wa taasisi ya Filbert Bayi Schools.


Kwa upande wake, Bayi alielezea kusikitishwa na tuhuma hizo, ambazo zinatolewa na mtu ambaye hajui kitu kuhusiana na Olimpiki, hivyo hawezi kujibizana naye, bali atamfikisha mahakamani.

“Mimi ni mtu niliyefanya mambo mengi kwenye jamii na ninaheshimika, sana sana nitamfikisha mahakamani akathibitishe, hawezi kunichafua hivihivi,” alisisitiza.


Gidabuday alipotafutwa kwa njia ya simu kuhusu kitisho cha Bayi kwenda mahakamani, alisema hatishiki na hilo yupo tayari kutetea hoja zake, akimtaka Bayi atangulie ili mengi zaidi yakaanikwe.


“Mimi si mtu wa uzushi, siwezi kukurupuka, kama anataka aende mahakamani itakuwa vizuri sana ili mengi zaidi yakaibuliwe, atangulie nitamkuta huko,” alisema Gidabyday kwa kujiamini


EmoticonEmoticon