BAADA YA KUICHAPA TOTO BAO 2 HIYO JANA,LEO NI ZAMU YA EXPRESS YA UGANDA UWANJA WA KAMBARAGE



Kikosi cha Simba kilicho ziarani Kanda ya Ziwa


BAADA ya jana kuichapa Toto African ya Mwanza mabao 2-0 katika mechi ya kirafiki iliyofanyika Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, mabingwa wa Tanzania, Simba SC leo wanashuka tena dimbani kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga kumenyana na mabingwa wa Uganda, Express ‘Tai Mwekundu.
 
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga  akiongea kwa njia ya simu leo asubuhi amesema kwamba tayari wako njiani kuelekea Shinyanga baada ya mechi ya jana dhidi ya Toto.
 
Katika mchezo wa jana, Wekundu wa Msimbazi walianza pambano hilo kwa kasi na iliwachukua dakika 17 tu kuandika bao la kwanza lililowekwa kimiani na Uhuru Selemani aliyemalizia vizuri pasi ya Abdallah Juma.
 .
Katika kipindi cha pili, Simba ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Abdallah Seseme na Hassan Khatib na nafasi zao kuchukuliwa na William Lucian (Gallas) na Jonas Mkude na mabadiliko hayo yalizaa matunda kwani katika dakika ya 48, Simba iliandika bao la pili lililofungwa na Salim Kinje mchezaji mpya wa Simba aliyesajiliwa kutoka AFC Leopards ya Kenya.
 
Salim Kinje alifunga bao hilo akiunganisha moja kwa moja kutoka nje ya 18 pasi ya kichwa kutoka kwa Uhuru Selemani.
 
Katika pambano la jana, wachezaji waliosajiliwa msimu huu walikuwa ni Waziri Hamad, Paulo Ngalema, Kiggi Makassy, Kinje na  Abdallah Juma.
 
Wachezaji wawili wa kikosi cha vijana Simba maarufu kwa jina la U-20, Haruna Chanonga na Lucian pia walicheza mechi yao ya kwanza kwa kikosi cha wakubwa.
 

SIMBA; Waziri, Hassan (Gallas), Ngalema (Omar Waziri), Obadia Mungusa, Haruna Shamte, Amri Kiemba (Edward Christopher), Chanonga, Seseme (Kiggi), Abdallah (Ramadhani Salum), Kinje na Uhuru.
Wakati huo huo: Kocha Mkuu wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic anatarajiwa kutua wakati wowote kuanzia sasa kutoka nyumbani, Serbia alikokuwa kwa mapumziko.


EmoticonEmoticon