RADIO 5 WAPOKEA KICHAPO

Zile tambo za muda mrefu kati ya Radio 5 na Sunrise Radio zote za Arusha kunako kabumbu zimemalizika jana katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid baada ya Radio 5 kupokea kichapo cha goli 4-2 kutoka kwa wababe wao Sunrise Radio.

      Radio 5 ndo walikuwa wa kwanza kuona lango la wapinzani wao kunako dakika ya 5 tu ya mchezo na dakika kumi baadae Sunrise Radio walisawazisha kupitia kwa kiungo wao machachari ambae ni captain Ibrahim Jamali kwa shuti kali lililomshinda golikipa wa Radio 5 na kujaa kimiani.

      Kabla ya kwenda mapumziko Radio 5 walicharuka kutafuta goli lakini ulinzi wa Sunrise Radio ulikuwa imara ukiongozwa na Ezra Agora(BBV) akisaidiana na Gasper Sambweti,kunako dakika ya 39 Sunrise Radio waliwainua washabiki wao vitini baada ya kutokea gonga safi kati ya Rodgers,Mussa Kinkaya na Ibrahim Jamal na hatimaye muuaji wa goli la kwanza Ibrahim Jamal hakufanya ajizi akapeleka tena kilio kwa Radio 5 kwa kupachika goli la 2,hadi mapumziko Sunrise 2,Radio 5 1

       Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikilisakama lango la mwenzake,mabadiliko yaliyofanywa na Sunrise Radio yalizaa matunda baada ya kumtoa Gasper Sambweti na kumwingiza Sele umande na kunako dakika ya 20 ya kipindi cha pili mshambuliaji hatari wa Sunrise Radio Mussa Kinkaya aliiandikia Sunrise Radio goli la 3 kwa njia ya kichwa baada ya kupokea krosi safi iliyochongwa na Ibrahim Jamal.

          Dakika ya 25 ya kipindi cha pili Sunrise Radio walifanya mabadiliko na kumtoa Joseph Amani na kumwingiza Hamis Abtway na kukabidhiwa nambari 2 na hatimaye Sele Umande kupanda mbele kuongeza mashambulizi na kunako dakika ya 35 ya kipindi cha pili Mussa Kinkaya tena aliiandikia Sunrise Radio goli la 4.

        Kwa upande wao Radio 5 wamekiri kwamba Sunrise Radio wapo juu kila idara ndani na nje ya studio na kusema kuwa wanastahili pongezi kwani wao ni bora kwa sasa na hakuna wa kupambanishwa nao kwa sasa.

      Kufuatia ushindi huo Sunrise Radio wamezawadiwa sh.laki tano(500,000)kutoka kwa bodi ya Wakurugenzi kama zawadi ya ushindi wa jana na kudai huo ni mwanzo tu mambo mengi mazuri yapo yanakuja kwa vijana wao.


EmoticonEmoticon